Waziri Mgalu amuita Dodoma mkandarasi anayesuasua

0
10


 

By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Hai. Naibu Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Subira Mgalu ameitahadharisha  kampuni ya Urban and Rural Engineering Services LTD inayotekeleza mradi wa umeme mkoani Kilimanjaro kwa kusuasua katika utendaji kazi, kuwataka watendaji wake kwenda mjini Dodoma kutoa maelezo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 25, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa wilayani Hai na kubainisha kuwa katika maeneo 83 ya kupeleka umeme kwa gharama ya Sh12 bilioni, hadi sasa amesambaza nishati hiyo katika maeneo 15, licha ya kuitwa na viongozi wa Serikali amekuwa akikaidi.

“Mkandarasi anatikisa kiberiti kujua kama kina njiti au hakina. Naomba nikwambie kiberiti kina njiti na kitawaka, ulichokifanya ni dharau na sasa unatupelekea kufanya uamuzi ya mapitio kwa kuwa sasa nathibitisha umeshindwa kazi,” amesema Subira.

Mgalu ameuagiza uongozi wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) mkoani Kilimanjaro kumtaka mkandarasi huyo kwenda mjini Dodoma pamoja na viongozi wa Rea kufanya mapitio, taratibu za kisheria zichukuliwe.

“Naagiza mkandarasi aende Dodoma tufanye mapitio na kuchukua taratibu za kisheria ili kama ameshindwa Serikali imkabidhi mkandarasi mwingine au tuwape Tanesco,” amesema.

Awali, mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alimtuhumu mkandarasi huyo kushindwa kazi na kusababisha wananchi kutoa malalamiko kila wakati kutokana na kutofikishiwa huduma ya nishati hiyo katika maeneo yao.

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here