Viongozi 53 serikalini wahudhuria mafunzo ya uongozi

0
54


By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Far es Salaam. Viongozi 53 wa Serikali na taasisi zake wanahudhuria kozi fupi ya mafunzo ya uongozi itakayotolewa kuanzia leo Februari 11 mpaka Ijumaa ijayo lengo likiwa ni kuwajengea uwezo.

Wanaohudhuria mafunzo hayo ni wakuu wa mikoa (7), katibu mkuu na naibu katibu mkuu (2), makatibu tawala wa mikoa (2), maofisa wa vyombo vya usalama (5), wakuu wa taasisi za umma (5), ofisa wa Takukuru (1), maofisa wa Bunge (20), maofisa kutoka Zanzibar (3) na watumishi wengine kutoka nchi za jirani.

Akizungumzia mafunzo hayo leo Jumatatu Februari 11, 2019 Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Luteni Jenerali Paul Massao amesema kozi hiyo ya siku tano itakuwa na moduli tatu zitakazowajengea uwezo kwenye masuala ya uongozi wa Taifa, ulinzi na usalama wa Taifa na menejimenti ya uongozi wa umma.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa viongozi, ndiyo maana kwa kuzingatia ushauri wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba mafunzo haya yatolewe mara mbili kwa mwaka. Tunatarajia Agosti mwaka huu tutakuwa na kozi nyingine kama hii,” amesema Massao.

Mkuu huyo wa chuo amesema mafunzo hayo yamezingatia maeneo mbalimbali ya kimkakati ambayo yatawaimarisha wanafunzi wa kozi hiyo ya sita yanayotolewa NDC. Amesema kauli mbiu ya mafunzo hayo ni “Uzalendo mhimili wa usalama wa Taifa”.

Akifungua kozi hiyo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama ameipongeza NDC kwa kuandaa mafunzo hayo kwa sababu yanalenga kuimarisha utendaji serikalini.

Ametoa wito kwa chuo hicho kushirikisha watu wengi zaidi kwenye mafunzo hayo ili matokeo yakawe makubwa serikalini. Pia, amewashauri wakuu wa mikoa kufikiria kuanzisha mafunzo kama hayo kwenye mikoa yao.

“Washiriki wote wa mafunzo haya nanyi mkahakikishe tunaona tofauti katika utendaji wenu. Mfikishe pia elimu mtakayoipata kwa wenzenu katika maeneo yenu ya kazi,” amesema Mhagama.

Wakuu wa mikoa wanaohudhuria mafunzo hayo ni pamoja na mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, Adam Malima (Mara), Robert Gabriel (Geita), Martin Shigela (Tanga) na Marco Gaguti (Kagera).

Viongozi hao wameonyesha kufurahia kozi hiyo huku wakitarajia itawaongezea ufanisi katika majukumu yao ya kila siku ya kiuongozi kama wakuu wa mikoa na kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama za mikoa yao.

“Kozi hii ni muhimu sana kwangu, natarajia itaniongezea maarifa zaidi katika utumishi wangu serikalini. Nitahakikisha ninawapatia wengine ujuzi ambao nitaupata hapa,” amesema Gaguti, mkuu wa mkoa wa Kagera.

 

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here