Vatican inaangalia uwezekano wa kuwafanya makasisi wanaume waliooa katika maeneo ya mbali ya Amazon

0
26


Haki miliki ya picha
AFP/Getty Images

Kanisa Katoliki limekuja na wazo la kuwafanya wanaume waliooa kuwa makasisi katika maeneo yanayozunguka mto Amazon, barani Amerika Kusini.

Maeneo hayo ambayo ni mbali, na yapo katikati ya msitu mnene, yana uhaba mkubwa wa makasisi, na bara la Amerika Kusini lina wafuasi wengi wa Ukatoliki.

Iwapo suala hilo litapitishwa, itakuwa ni mabadiliko makubwa ndani ya kanisa hilo kwa kipindi cha miaka 1000.

Mabadiliko hayo yamependekezwa kwenye Waraka muhimu wa Mazingira wa Papa – Laudato Si – uliochapishwa mwaka 2015.

Katika waraka huo, Papa Francis, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ameandika kuwa, eneo hilo la Amazon linakabiliana na na changamoto ambazo (kuzitatua) “inahitaji mabadiliko ya kimfumo na kibinafsi kwa watu wote, mataifa yote (ya eneo hilo la Amazon) pamoja na Kanisa.”

Waraka huo unatarajiwa kujadiliwa kwa marefu na mapana kwenye mkutano maalumu wa majimbo ya kanisa hilo kwenye eneo lote la msitu wa Amazon mwezi Oktoba mwaka huu jijini Roma, Italia.

Mkutano huo utahudhuriwa na Maaskofu na wawakilishi wa waumini wa eneo hilo ambalo linapatikana katika nchi za Brazil, Bolivia, Peru, Ecuador, Colombia, Venezuela, Guyana, Suriname na French Guyana.

Eneo hilo lina wakazi takribani milioni 33 na ni chanzo muhimu cha maji safi (moja ya tano ya dunia), hewa safi ya oksijeni (moja ya tano ya dunia) na moja ya tatu ya hifadhi ya misitu duniani.

Vatican inasema eneo hilo hata hivyo linaibua changamoto kubwa ya kikasisi na kimazingira – lakini ni uhaba wa makasisi ambao Kanisa linaweza kupata ufumbuzi wake wa moja kwa moja.

Haki miliki ya picha
Reuters

Image caption

Je, Papa Francis ni mwanamageuzi anayelibadili Kanisa?

Katika kuliendea hilo, Waraka wa Papa wenye kurasa 45 ambao uliandaliwa kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na Maaskofu na na jamii husika, unashauri kuwa Mkutano wa mwezi Oktoba uangalie uwezekano wa kuwafanya makasisi, wanaume amabo ni watu wazima, na wanaoheshimika kwenye jamii zao.

Waraka unawataja kuwa “wanaume wenye tabia njema iliyothibitika” kama suluhu ya uhaba wa makasisi – na kutaja kuwa lazima wawe watu wa kipekee kwenye jamii ya Kikatoliki na wenye familia ambazo tayari zimetanuka.

Waraka huo pia bila kutoa ufafanuzi pia unashauri kuwa wanawake wapewe baadhi ya kazi za kikasisi.

Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, yatabadili kwa mara ya kwanza maamuzi ya Mabaraza mawili ya Lateran ya mwaka 1123 na 1139 ambayo yalipiga marufuku makasisi kuoa – hivyo, ni kwa takriban miaka 1,000 sasa kanisa limeshikilia msimamo wa useja kwa makasisi.

Kuondoa uwezekano wa ndoa katika kipindi hicho kulihakikisha kuwa watoto ama wake wa makasisi wasingetaka kupewa mali za makasisi hao pindi watakapofariki, ambazo moja kwa moja zilimilikiwa na kanisa.

Huwezi kusikiliza tena

Tazama Papa Francis alivyowazuia waumini kuibusu pete yake

Ilichukua karne kadhaa kwa kiapo cha useja kutekelezwa, na baadae kuwa jambo la kawaida kwa makasisi wa kanisa hilo.

Mwisho wa mkutano huo, washiriki watapigia kura vipengele kadhaa vya waraka ulioboreshwa, na kisha mapendekezo yao kurejeshwa kwa Papa.

Papa baada ya kupata maoni hayo ataamua iwapo ayapitishe kwa kuyafanya maamuzi rasmi ya kanisa ama la.

Kwa hakika suala hililitaendeleza mjadala ndani na nje ya Kanisa Katoliki iwapo Papa Francis ni mwana mabadiliko, ambaye anapambana kulibadilisha Kanisa.

Mwaka2013, alizungumzia juu ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutokubaguliwa kwenye jamii.

“Kama mtu ni mpenzi wa jinsia moja na anamsaka Mungu na ana nia njema, mimi ni nani kumhukumu?” alisema.

  • Papa Francis awataka wahudumu wa saluni kuacha udaku
  • Vatican yapinga dhana ya mapenzi ya jinsia moja

Baadhi ya watu walikaribisha kauli hiyo, wakidhani kuwa ilikuwa ni alama ya Papa kutaka kubadili msimamo – lakini, akatoka wazi na kusimamia msimamo wa Ukatoliki kuwa vitendo vya mahusiano yajinsia moja ni dhambi, japo akasema iwapo mtu ana maumbile ya tofauti si dhambi.

Mwaka 2009, Kanisa lilitoa ruhusa maalum kwa makasisi wa Kianglikana waliooa kujiunga na Ukatoliki na kubakia na nafasi zao.

Uamuzi huo ulilenga kuwapokea makasisi wahafidhina wa Kianglikana mabao kipindi hicho walikuwa wakipinga kanisa lao kukubali wanawake kuwa makasisi.

Ukasisi ndani ya Kanisa Katoliki unafanywa na Wanaume tu.

Waraka wa Amazon ukipita, utaupa nguvu mpya mjadala huu wa miaka mingi.

Na yapasa kukumbuka kuwa, alipoulizwa mwezi Januari mwaka huu juu ya kuwafanya makasisi wanaume waliooa, Papap Francis alisema binafsi anapingana na mabadiliko yoyote kwenye Ukasisi.Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here