Mwili wa Etienne Tshisekedi kuwasili DRC leo

0
67


 

DRC. Mwili wa kiongozi wa upinzani, Etienne Tshisekedi ambaye ni baba wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), Felix Tshisekedi unatarajiwa kuwasili nchini humo leo, ikiwa ni miaka miwili baada ya kifo chake.
Kulingana na familia, mwili huo utawasili kutoka nchini Ubelgiji kwa mazishi.
Tshisekedi alifariki mjini Brussels akiwa na umri wa miaka 84 Februari 2017 lakini mwili wake ulisalia katika mji huo wa Ubelgiji kutokana na wasiwasi wa kisiasa kwa utawala wa rais wa zamani wa taifa hilo, Joseph Kabila.
Mazishi yake yatafanyika katika Viwanja vya Mashahidi, kulingana na nduguye, Askofu Gerard Mulumba.
Mulumba anasema kuwa baada ya kuukaribisha mwili katika uwanja wa ndege utasafirishwa hadi katika uwanja huo kwa maombolezi.
Amesema kuwa tayari maandalizi katika uwanja huo ikiwemo ujenzi wa jukwaa umekamilika mbali na yale ya maofisa wa polisi ambao wataongoza gwaride ili kumpatia heshima za mwisho baba huyo wa upinzani DRC.
Takriban marais watano wa bara la Afrika wamethibitisha kuhudhuria mazishi yake.

Kuzikwa kama shujaa
”Ni zaidi ya miaka miwili tangu tulipoanza kutumia kila njia kuusafirisha mwili wake” , alisema Mulumba akinukuliwa na BBC.
Akiwa mwanasiasa wa muda mrefu, Tshisekedi alihudumu katika upinzani kwa miongo kadhaa lakini hakufanikiwa kuiongoza nchi hiyo, kikombe ambacho kimemwangukia mwanaye, Felix.
Akiwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa zamani wa DRC, Mobutu Sese Seko, Tshisekedi alianzisha chama cha Union for Democracy and Special Progress (UDPS) mwaka 1982 baada ya kuachiliwa kutoka jela.
Utawala wa Kabila
Mwaka 1997, baada ya Mobutu kung’atuliwa madarakani na kundi lililoongozwa na Laurent Kabila (Baba wa Joseph Kabila), Etienne Tshisekedi alianza kuwa mpinzani wa utawala mpya, msimamo aliokuwa nao hata baada ya mauaji ya Kabila 2001, huku mwanawe Joseph akishika uongozi.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2011 uliodaiwa kukumbwa na udanganyifu , Tshisekedi alikataa kutambua utawala wa Kabila hadi kifo chake.
Miaka miwili baada ya kifo chake, Januari 24, mwanawe Felix Tshisekedi aliapishwa kuwa rais baada ya uchaguzi ambao ulimfanya Kabila kuondoka madarakani baada ya miaka 18.
Uchaguzi huo, hata hivyo, ulikumbwa na madai mengi ya udanganyifu huku siasa za taifa hilo bado zikitawaliwa na Kabila ambaye alijipatia umaarufu mkubwa akiwa madarakani.
Siku ya Jumatatu Rais Tshisekedi alimteua mwanasiasa wa muda mrefu, Sylvestre Ilunga Ilunkamba kuwa waziri mkuu.

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here