Mvua yaleta adha Mwanza, yasomba bidhaa za wafanyabiashara

0
3


Salvatory akimsaidia mwenzake Simon asisombwe

Salvatory akimsaidia mwenzake Simon asisombwe na maji wakati wakifuata mapipa yaliyosombwa na maji eneo la mto Mirongo mtaa wa Uhuru jijini Mwanza kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha. Picha na Jesse Mikofu 

By Sada Amir na Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa moja mchana leo Ijumaa  Oktoba 18, 2019 imesababisha madhara jijini Mwanza nchini Tanzania ikiwemo bidhaa za wafanyabiashara zilizopangwa kwenye mabaraza ya maduka kusombwa na maji.

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha kuanzia saa 7:45 mchana hadi saa 9:14 alasiri pia imesababisha msongamano wa magari katika barabara ya Nyerere baada ya barabara ya Uhuru kufungwa kutokana na maji kupita juu ya daraja la mto Mirongo.

Wafanyabiashara walioathirika zaidi ni wenye maduka ya jumla na rejereja katika mitaa ya Liberty na Uhuru ambao bidhaa zao zimesombwa na maji ya Mto Mirongo uliojaa hadi kupita juu ya daraja.

Miongoni mwa bidhaa zilizosombwa na maji ya mto huo unaomwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria ni pamoja na mapipa matupu, mabeseni, ndoo, malapa/yeboyebo na madumu ya mafuta ya kupikia.

Mwananchi pia imeshuhudia bidhaa za wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga zikiwemo vikapu, vinyago mapambo na vitu vingine vya asili vikisombwa na maji ya Mto huo.

Mto Mirongo unaokatisha katikati ya jiji la Mwanza hukusanya maji yake kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu na Misungwi.

AdvertisementKwa wilaya ya Nyamagana, maji ya mto huo yanatoka maeneo ya Igoma, Mabatini na Kishili kwa Jiji la Mwanza huku maji mengine wakati kwa Magu maji hayo hutokea maeneo ya Kisesa.

Justine Mashimba, mfanyabiashara wa duka la jumla mtaa wa Liberty ameiambia Mwananchi kuwa anaendelea kufanya tathmini ya mali iliyosombwa na maji kabla ya kutoa taarifa kamili ya hasara iliyotokana na mvua hiyo.

“Tumefanikiwa kuokoa baadhi ya mapipa ingawa sehemu kubwa hatuwezi kutokana na nguvu ya maji na hofu ya kuzama; nimetuma vijana kukimbilia ziwani kuona kama tunaweza kupata yatakayopelekewa huko kutokana na mto huu kumwaga maji yake ziwani,” amesema Mashimba

Katika tukio lingine lililotokea Oktoba 17, 2019, bidhaa za wafanyabiashara katika soko kuu la muda jijini Mwanza eneo la Mbugani ziliharibika baada ya kulowa kutokana na miundombinu ya mibovu ya soko hilo.

Bidhaa za wafanyabiashara hao zimelowa kutokana na paa la vibanda vyao vya biashara kuwa fupi na hivyo kusababisha maji kumwagikia kwenye meza walizopanga bidhaa.

Walioathirika zaidi ni wafanyabiashara wa nafaka akiwemo Eva Urassa anayeuza dengu, kunde, maharagwe, mchele na karanga.

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Kilomoni Kibamba amesema ofisi yake tayari imemwagiza mkandarasi anayejenga vibanda na kuta za soko hilo la muda kufanya marekebisho ya kasoro zilizobainika ifikapo Oktoba 21, 2019.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema ofisi yake inaendelea kukusanya taarifa na kufanya tathmini kujua madhara yaliyotokana na mvua hizo kabla ya kutoa taarifa kamili.

“Kwa sasa sina taarifa; ngoja nifuatilie kujua madhara ndipo nitakapozungumzia madhara ya mvua,” amesema Mongella

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro hakupatikana kuzungumzia iwapo kuna madhara kutokana na mvua hizo baada ya simu yake ya kiganjani kuita muda mrefu bila kujibiwa.

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here