Muumini alivyookoa wenzake kwa kumtimua aliyeshambulia

0
22


 

 Wakati Abdul Aziz, mkimbizi kutoka Afghanistan, alipoona mtu aliyekuwa ameshikilia bunduki nje ya msikiti wao jijini Christchurch, alikimbia kumfuata akiwa na silaha moja pekee aliyoweza kuipata, mashine ya kielektroniki ya malipo kwa kutumia kadi.
Watu saba waliuawa wakati gaidi huyo, anayeamini watu wenye ngozi nyeupe ni bora, alipoingia katika msikiti wa Linwood ambao ni mmoja kati ya misikiti miwili iliyoshambuliwa Ijumaa iliyopita wakati waumini wakipiga magoti kusali.
Lakini idadi ya watu waliofariki ingeweza kuwa kubwa zaidi kama si vitendo vya kishujaa vya Aziz, ambaye jitihada zake za kumsumbua na kumuondoa mtu huyo aliyekuwa na silaha zimemfanya asifiwe na watu mbalimbali.
“Huwezi kuwa na muda wa kutosha kufikiria, chochote unachofikiria unakifanya, unaelewa,” Aziz aliiambia AFP, akitaka asiitwe shujaa wakati Waislamu wa eneo hilo walipokuwa wakimininika kumshukuru kwa kuokoa ndugu zao.
Aziz na watoto wake wanne walikuwa wakisali kwenye msikiti huo wakati waliposikia mlipuko wa risasi nje ya jengo.
Awali walidhani kuwa kulikuwa na mtu alikuwa akifyatua baruti, lakini Aziz akawa na shaka na kukimbilia nje ya msikiti, akachukua mashine ndogo ya kielektroniki ya malipo ya kutumia kadi ya benki.
Nje ya jengo, alishtushwa kuona mtu aliyekuwa amevalia kama nguo za kijeshi.
“Kwanza, sikujua kama alikuwa mtu mzuri au mbaya. Lakini alipoanza kujiapiza, nilijua si mtu mzuri,” alisema.
Aziz alirusha ile mashine ndogo kuelekea kwa mtu huyo anayejulikana kama Brenton Tarrant na baadaye kukimbilia katikati ya magari kadhaa yaliyokuwa yameegeshwa, huku mshambuliaji huyo akimimina risasi kuelekeza kwake.
Baadaye Aziz akasikia mmoja wa watoto wake akiita “baba, tafadhali rudi ndani!”
Akiwa hajajeruhiwa na risasi hizo, Aziz aliokota bunduki iliyokuwa imetupwa na mtu huyo na akapiga kelele akisema “njoo huku” na kurudiarudia katika jitihada za kumfanya mtu huyo asielekee kwa watoto wake na waumini wengine.
“Alipoona bunduki mikononi mwangu, sijui kilichotokea nini. Aliidondosha bunduki aliyokuwa nayo na nikaanza kumfukuza nikiwa na bunduki yangu… nilifanikiwa kuirusha bunduki yangu na ikagonga dirisha, na niliweza kuona alikuwa amechanganyikiwa.”
Aziz aliendelea kumfukuza wakati Tarrant akiondoka na gari lake eneo hilo.
Baadaye Aziz, ambaye ana umri wa miaka 48, alirejea msikitini ambako alikuta miili ya watu waliouawa.
Aziz, ambaye sasa ni raia wa Australia, alihamia nchi hiyo akiwa mtoto. Aliishi Sydney kwa karibuni miaka thelathini kabla ya kuhamia Christchurch miaka michache baadaye.
Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern amesema leo Jumapili kuwa atataka majibu kutoka mtandao wa Facebook na mingine ya kijamii kuhusu iliwezekanaje shambulio lililoua karibu watu 50 lilirushwa moja kwa moja kwenye kurasa zao.
Akiamini kuwa kuna maswali “zaidi yanayotakiwa kujibiwa” na kampuni hiyo kubwa, Ardern alisema kiongozi wa uendeshaji wa Facebook, Sheryl Sandberg amekuwa akiwasiliana na “kukubali kilichotokea hapa New Zealand”.

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here