Mangula aeleza tofauti ya viongozi wakati wa Mwalimu Nyerere na sasa

0
6


 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Phillip Mangula amesema tofauti  ya viongozi wakati mwalimu Julius Nyerere alipokuwa rais wa waliopo sasa ni mafunzo ya jinsi ya kuongoza.

Mangula ameeleza tofauti hizo leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 katika mdahalo wa kumbukumbu ya miaka 20 ya  kifo cha Mwalimu Nyerere  uliofanyika Butiama mkoani Mara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Katika mdahalo huo ulioendeshwa na mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na kurushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ulitoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali kwa viongozi wastaafu waliowahi kufanya kazi na Nyerere.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye aliuliza tafauti ya mfumo wa uongozi katika chama na Serikali ulikuwepo wakati Nyerere alipokuwa Rais wa Tanzania na uongozi wa sasa.

“Mwalimu Nyerere wakati anaongoza naona watu walikuwa wamenyooka sana, kuna tofauti gani kati ya wakati ule na wakati huu hasa kwenye Chama na Serikali,” amesema Kiboye.

Akijibu swali hilo Mangula amesema, “tofauti ipo, kama nilivyosema Mwalimu aliamini katika masomo kwa viongozi kwa sasa hawaendi kwenye masomo.”

Advertisement



“Kwa hiyo kila mtu anaenda kwa utaratibu wake anabuni mwenyewe namna ya kuendesha shughuli zake hakuna utaratibu wa pamoja wa namna kuchukua mafunzo.”

Huku akicheka Mangula amesema Mwalimu Nyerere alisisitiza mafunzo ya vitendo kwa viongozi kuliko nadharia.

“Alikuwa anasema msiwafundishe tu nadharia viongozi waende wakakae vijijini, hivyo walikuwa wanaenda vijijini wanakaa mwezi mzima na wananchi,” amesema Mangula.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo naye aliuliza swali akitaka kujua sababu Mwalimu Nyerere kutaifisha shule.

Katika majibu yake Mangula amesema lengo la Mwalimu Nyerere kutaifisha shule lilikuwa ni kujenga utaifa.

“Moja alikuwa ana jitihada za kujenga utaifa maana shule zilikuwepo za Wazungu, Waasia na tuligawanywa katika makundi kwa wanafunzi waliomaliza shule mbalimbali, akaamua hapana hebu tuondoe hii, akataifisha zile shule zote zikawa za Taifa, wote wanatoka popote wanaenda kusoma popote,” amesema Mangula.

Mdahalo huo uliwashirikisha wananchi na viongozi waliofanya kazi na Mwalimu wakielezea uzoefu wao na mambo waliyojifunza katika uongozi wake.





Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here