Majaliwa: Serikali inaendelea kutafuta masoko ya tumbaku

0
36


 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Tabora. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta masoko ya tumbaku ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi na kuinua kipato.

Ameyasema hayo leo Jumapili Julai 14, 2019 wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku kutoka mikoa mbalimbali katika mkutano uliofanyika mkoani Tabora.

Amebainisha tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na nchi mbalimbali zikiwemo Vietnam na Misri iliyoahidi kuisaidia Tanzania kupata wanunuzi.

Amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni zinazonunua tumbaku nchini ili ziongeze kiwango cha ununuzi kuwawezesha wakulima kuzalisha zaidi.

“Wakulima wanahitaji kuzalisha zaidi lakini wanakwamishwa na kiwango wanachowekewa (ukomo wa uzalishaji) na wanunuzi ambacho ni kidogo ukilinganisha uwezo wa wakulima katika kuzalisha zao hilo,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) ili iendelee na ununuzi wa zao hilo.

Amesema awali kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa wanunuzi wa tumbaku nchini ilitoa kusudio la kutaka kuacha kununua zao hilo.

Kiongozi huyo amebainisha Serikali inashirikiana na nchi ya Malawi katika utafutaji wa masoko ya zao hilo na tayari kampuni za Malawi zimeahidi kununua tumbaku nchini.

Source link

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here